Haturuhusiwi kamwe kutumia neno "Mungu" na neno "bahati" katika sentensi moja; kwani Mungu hatubahatishi, anatubariki. Ukitumia neno "Mungu" na neno "bahati" katika sentensi moja umevunja Amri Kuu ya Kwanza ya Mungu; isemayo, "Usiwe na miungu mingine ila mimi." Ukifanya hivyo, umemwabudu mungu mwingine aitwaye "bahati". Hatupaswi asilani kusema, "Mungu amenipa bahati ya kuuona mwaka mpya". Tunapaswa kusema, "Mungu amenibariki kuuona mwaka mpya." Kila jambo linalotokea katika maisha hutokea kwa makusudi maalumu, kutokana na sheria ya ulimwengu wa roho iitwayo Chanzo na Matokeo, na lilishapangwa tayari na Mwenyezi Mungu litokee. Jambo jema likikutokea hiyo si bahati. Hiyo ni baraka. Kwa hiyo, hupaswi kusema una bahati, unapaswa kusema umebarikiwa. Kuna watu badala ya kumtegemea Mungu wanategemea bahati! Usitegemee bahati. Tegemea baraka, kwani baraka hutoka kwa Mungu. Yupo mtu ambaye hajasoma sana lakini ni mkurugenzi wa kampuni, na yupo mtu ambaye amesoma sana lakini ni karani wa kampuni. Katika muktadha huo wa kazi, mmoja kati ya hawa amebarikiwa kwa kiwango chake, mwingine amebarikiwa kwa kiwango kingine. Jitihada inapokutana na fursa kisha jambo fulani zuri likakutokea katika maisha yako, jambo hilo lilishapangwa na Mungu karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwako. Hiyo si bahati, ni haki yako. Kama ulipangwa kutofanikiwa hutafanikiwa asilani! Kwani Mungu alijua hutaweza kuutumia uwezo aliokupa wa kukufanya ufanikiwe; na yeye hawezi kukulazimisha uutumie uwezo huo au la, kwa kuwa una uhuru wa kuchagua mafanikio au umaskini. Ulimwengu wetu una sheria zake, zijulikanazo kama sheria za asili. Ulimwengu wa roho una sheria zake pia, zijulikanazo kama sheria za ulimwengu wa roho. Sheria ya ulimwengu wa roho ijulikanayo kama Mizizi na Matawi, au Chanzo na Matokeo, ndiyo inayosababisha kila kitu kinachotokea hapa ulimwenguni kiwe na sababu maalumu kutoka katika ulimwengu wa roho; isipokuwa "bahati" au baraka. Soma zaidi hapa: https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=2327290233961458&id=100000415120038 #hochma #masach #bahati #luck https://www.instagram.com/p/BtcBhEsn-a8/?utm_source=ig_tumblr_share&igshid=t0dttevch92p











