Fedha ni mtumishi mzuri sana wa maisha ya watu, lakini ni bosi mbaya sana wa maendeleo ya maisha yao. Acha fedha iwe mtumishi mzuri sana wa maisha yako, lakini wewe uwe bosi mzuri sana wa maendeleo ya maisha yako, hususan kwa kuzingatia bajeti na akiba ya mapato yako. Katika nukuu ya leo ninakupa vidokezo vya usimamizi wa fedha. Yaani, jinsi ya kuandaa bajeti na jinsi ya kuweka akiba. Akiba ni jambo la muhimu sana katika maisha ya mtu. Lazima uhakikishe kuwa unaweka fedha kando, angalau kidogo, kila mwezi kwa ajili ya maendeleo ya maisha yako. Tatizo hata hivyo ni kwamba watu wengi hawana utamaduni wa kuandaa bajeti na kuweka akiba. Kusema ukweli, watu wengi huishi mshahara kwa mshahara. Yaani, mapato wanayoyapata hayawatoshelezi kwa mwezi mzima. Mantiki ya kauli hiyo ni kwamba, kiasi chochote cha fedha wanachokipata huenda moja kwa moja kwenye kulipa madeni; na aghalabu huwa hawabaki na kitu. Kwa hiyo, hakuna mtiririko mzuri wa fedha wa kuwawezesha kuweka akiba – kwa ajili ya matumizi mengine ya kawaida, au kwa ajili ya dharura. Kama unaishi kwa njia ya mshahara kwa mshahara, basi jua kuwa umekwama katika mtego wa mbio za panya. Maana yake ni kwamba abadani hutaweza kuendelea katika maisha yako. Mbio za panya ni hali ya watu kutafuta maisha bora kwa nguvu zao zote, lakini hatimaye wanaambulia patupu. Watu wengi wanaoishi ughaibuni, kwa mfano Amerika au Ulaya, wanaishi katika mitego ya mbio za panya. Wanaishi mishahara kwa mishahara. Si matajiri wala si maskini. Wako katikati. Lakini, suluhisho pekee la kuishi nje ya mtego wa mbio za panya ni kuandaa bajeti na kuweka akiba. Kabla hata ya kuwa na mawazo ya kuwekeza fedha mahali, kwa ajili ya manufaa ya baadaye, unahitaji kwanza kuhakikisha kuwa unazisimamia fedha hizo vizuri na unaandaa bajeti ya matumizi yake. Bajeti ni njia ya kutoa sadaka ya kitu fulani katika maisha yako, kwa ajili ya kitu kingine chenye manufaa zaidi. Soma zaidi hapa: https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=2795197717170705&id=100000415120038 #fedha #money #bajeti #budgetplanner #budget #akiba #savings https://www.instagram.com/p/B4KFS0uHAei/?igshid=t2vztf1bpbzv










